| Chapter 20 |
1 |
"Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake.
|
2 |
Akapatana nao kuwalipa dinari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba lake la mizabibu.
|
3 |
Akatoka mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi.
|
4 |
Akawaambia, `Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami nitawapeni haki yenu.`
|
5 |
Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo.
|
6 |
Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, `Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?`
|
7 |
Wakamjibu: `Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri.` Yeye akawaambia, `Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.`
|
8 |
"Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza hazina wake, `Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.`
|
9 |
Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakapokea kila mmoja dinari moja.
|
10 |
Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja.
|
11 |
Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnung`unikia yule bwana.
|
12 |
Wakasema, `Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia kazi ngumu kutwa na jua kali?`
|
13 |
"Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, `Rafiki, sikukupunja kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa denari moja?
|
14 |
Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.
|
15 |
Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je, unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?"`
|
16 |
Yesu akamaliza kwa kusema, "Hivyo, walio wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho."
|
17 |
Yesu alipokuwa anakwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia,
|
18 |
"Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu auawe.
|
19 |
Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe, apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa."
|
20 |
Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu.
|
21 |
Yesu akamwuliza, "Unataka nini?" Huyo mama akamwambia, "Ahidi kwamba katika Ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto."
|
22 |
Yesu akajibu, "Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?" Wakamjibu, "Tunaweza."
|
23 |
Yesu akawaambia, "Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu."
|
24 |
Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia hao ndugu wawili.
|
25 |
Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, "Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu na wakuu hao huwamiliki watu wao.
|
26 |
Lakini kwenu isiwe hivyo, ila yeyote anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote;
|
27 |
na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu.
|
28 |
Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi."
|
29 |
Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata.
|
30 |
Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!"
|
31 |
Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!"
|
32 |
Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, "Mnataka niwafanyie nini?"
|
33 |
Wakamjibu, "Mheshimiwa, tunaomba macho yetu yafumbuliwe."
|
34 |
Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata.
|