| Chapter 5 |
1 |
Ziko habari za kuaminika kwamba kuna uzinzi miongoni mwenu; tena ni uzinzi mbaya ambao haujapata kuwako hata kati ya watu wasiomjua Mungu. Nimeambiwa eti mmoja wenu anaishi na mke wa baba yake!
|
2 |
Mnawezaje kujivuna? Ingekuwa afadhali kwenu kuomboleza, na huyo aliyefanya kitu hicho aondolewe miongoni mwenu.
|
3 |
Nami, kwa upande wangu, ingawa kwa mwili niko mbali nanyi, hata hivyo kwa roho niko hapo pamoja nanyi: na hivyo, kama vile nipo hapo, nimekwisha mhukumu huyo aliyefanya jambo hilo la aibu.
|
4 |
Wakati mnapokusanyika pamoja kwa jina la Bwana Yesu, nami nikiwa pamoja nanyi kwa roho, basi, kwa uwezo wa Bwana wetu Yesu,
|
5 |
mkabidhini mtu huyo kwa Shetani ili mwili wake uharibiwe na roho yake iweze kuokolewa Siku ile ya Bwana.
|
6 |
Majivuno yenu hayafai! Je, hamjui kwamba chachu kidogo huchachusha donge lote la unga?
|
7 |
Jitakaseni, mkatupe mbali chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu kama mnavyopaswa kuwa; maana, Kristo, Pasaka yetu, amekwisha tolewa tambiko.
|
8 |
Basi, tufanye karamu hiyo si kwa chachu ile ya kale, chachu ya ubaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, mkate wa usafi na kweli.
|
9 |
Niliwaandikia katika barua yangu msishirikiane na wazinzi.
|
10 |
Ukweli ni kwamba sikuwa na maana ya watu wote duniani walio wazinzi, wachoyo, walaghai na wenye kuabudu sanamu. Maana, ili kuwaepa hao wote ingewalazimu ninyi kuihama dunia hii kabisa!
|
11 |
Nilichoandika ni hiki: msishirikiane na ndugu Mkristo aliye mzinzi, mchoyo, mwenye kuabudu sanamu, mchongezi mlevi na mlaghai. Mtu wa namna hiyo, hata kula msile naye.
|
12 |
Je, ni shauri langu kuwahukumu watu walio nje? Hao Mungu atawahukumu. Je, ninyi hampaswi kuwahukumu wale walio katika jamii yenu ninyi wenyewe?
|
13 |
Mfukuzeni mbali nanyi huyo mwovu!
|