| Chapter 4 |
1 |
Nanyi wakuu, watendeeni watumwa wenu kwa uadilifu na haki, mkikumbuka kwamba nanyi pia mnaye Bwana mbinguni.
|
2 |
Dumuni katika sala, na mnaposali muwe waangalifu, mkimshukuru Mungu.
|
3 |
Vilevile, mtuombee sisi pia ili Mungu atupe fursa ya kuuhubiri ujumbe wake kuhusu siri ya Kristo. Kwa ajili hiyo mimi niko sasa kifungoni.
|
4 |
Basi, ombeni ili niweze kusema kama inavyonipasa na kwa namna itakayodhihirisha siri hiyo.
|
5 |
Muwe na hekima katika uhusiano wenu na watu wasioamini, mkitumia vizuri kila nafasi mliyo nayo.
|
6 |
Mazungumzo yenu yanapaswa kuwa daima mema na ya kuvutia, na mnapaswa kujua jinsi ya kumjibu vizuri kila mmoja.
|
7 |
Ndugu yetu mpenzi Tukiko, mfanyakazi mwaminifu na mtumishi mwenzetu katika kazi ya Bwana, atawapeni habari zangu zote.
|
8 |
Ndiyo maana namtuma, ili aichangamshe mioyo yenu kwa kuwaambieni habari zetu.
|
9 |
Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpenzi na mwaminifu, ambaye ni mwananchi mwenzenu. Watawapeni habari za mambo yote yanayofanyika hapa.
|
10 |
Aristarko, ambaye yuko kifungoni pamoja nami, anawasalimuni; hali kadhalika Marko, binamu yake Barnaba, (mmekwisha pata maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni).
|
11 |
Naye Yoshua aitwaye Yusto, anawasalimuni. Miongoni mwa Wayahudi waliokwisha pokea imani, hawa tu peke yao, ndio wanaofanya kazi pamoja nami kwa ajili ya Utawala wa Mungu; nao wamekuwa msaada mkubwa kwangu.
|
12 |
Epafra, mwananchi mwenzenu na mtumishi wa Kristo Yesu anawasalimuni. Daima anawaombeeni ninyi kwa bidii ili mpate kusimama imara, mkomae na kuwa thabiti kabisa katika mambo yote anayotaka Mungu.
|
13 |
Naweza kushuhudia kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu na kwa ajili ya watu wa Laodikea na Hierapoli.
|
14 |
Luka, daktari wetu mpenzi, na Dema, wanawasalimuni.
|
15 |
Salamu zetu kwa ndugu zetu wa Laodikea; msalimuni dada Nimfa pamoja na jumuiya yote ya waumini inayokutana nyumbani kwake.
|
16 |
Mkisha soma barua hii, hakikisheni kwamba inasomwa na Wakristo wa Laodikea; na ninyi fanyeni mpango mpate kuisoma barua waliyoipata kwao.
|
17 |
Mwambieni Arkipo aitekeleze vizuri ile huduma aliyokabidhiwa na Bwana.
|
18 |
Naandika haya kwa mkono wangu mwenyewe: Salamu kutoka kwangu, mimi Paulo. Kumbukeni kwamba niko kifungoni. Neema ya Mungu iwe nanyi.
|