| Chapter 3 |
1 |
Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu.
|
2 |
watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu;
|
3 |
watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema;
|
4 |
watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu.
|
5 |
Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo.
|
6 |
Baadhi yao huenda katika nyumba za watu na huwateka wanawake dhaifu waliolemewa mizigo ya dhambi na ambao wanaongozwa na tamaa za kila aina;
|
7 |
wanawake ambao wanajaribu daima kujifunza lakini hawawezi kuufikia ujuzi wa huo ukweli.
|
8 |
Watu hao huupinga ukweli kama vile Yane na Yambre walivyompinga Mose.
|
9 |
Lakini hawataweza kuendelea zaidi kwa maana upumbavu wao utaonekana wazi kwa wote. Ndivyo ilivyokuwa kwa akina Yane na Yambre.
|
10 |
Wewe lakini, umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudi yangu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu, subira yangu,
|
11 |
udhalimu na mateso yangu. Unayajua mambo yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Lustra. Nilivumilia udhalimu mkubwa mno! Lakini Bwana aliniokoa katika mambo hayo yote.
|
12 |
Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe.
|
13 |
Watu waovu na wadanyanyifu watazidi kuwa waovu zaidi na zaidi kwa kuwadanganya wengine na kudanganyika wao wenyewe.
|
14 |
Lakini wewe dumu katika ukweli ule uliofundishwa, ukaukubali kabisa. Unawajua wale waliokuwa walimu wako.
|
15 |
Unakumbuka kwamba tangu utoto wako umeyajua Maandiko Matakatifu ambayo yaweza kukupatia hekima iletayo wokovu kwa njia ya imani kwa Kristo Yesu.
|
16 |
Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili,
|
17 |
ili mtu anayemtumikia Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila tendo jema.
|