| Chapter 10 |
1 |
Sheria ya Wayahudi si picha kamili ya mambo yale halisi: ni kivuli tu cha mema yanayokuja. Dhabihu zilezile hutolewa daima, mwaka baada ya mwaka. Sheria yawezaje, basi, kwa njia ya dhabihu hizo, kuwafanya wale wanaoabudu wawe wakamilifu?
|
2 |
Kama hao watu wanaomwabudu Mungu wangekuwa wametakaswa dhambi zao kweli, hawangejisikia tena kuwa na dhambi, na dhabihu hizo zote zingekoma.
|
3 |
Lakini dhabihu hizo hufanyika kila mwaka kuwakumbusha watu dhambi zao.
|
4 |
Maana damu ya fahali na mbuzi haiwezi kamwe kuondoa dhambi.
|
5 |
Ndiyo maana Kristo alipokuwa anakuja ulimwenguni, alimwambia Mungu: "Hukutaka dhabihu wala sadaka, lakini umenitayarishia mwili.
|
6 |
Sadaka za kuteketezwa au za kuondoa dhambi hazikupendezi.
|
7 |
Hapo nikasema: `Niko hapa ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako kama ilivyoandikwa juu yangu katika kitabu cha Sheria."`
|
8 |
Kwanza alisema: "Hutaki, wala hupendezwi na dhabihu na sadaka, sadaka za kuteketezwa na za kuondoa dhambi." Alisema hivyo ingawa sadaka hizi zote hutolewa kufuatana na Sheria.
|
9 |
Kisha akasema: "Niko hapa, ee Mungu, tayari kufanya mapenzi yako." Hivyo Mungu alibatilisha dhabihu za zamani na mahali pake akaweka dhabihu nyingine moja.
|
10 |
Kwa kuwa Yesu Kristo alitimiza mapenzi ya Mungu, sisi tunatakaswa dhambi zetu kwa ile dhabihu ya mwili wake aliyotoa mara moja tu, ikatosha.
|
11 |
Kila kuhani Myahudi humhudumia Mungu kila siku, akitoa dhabibu zilezile mara nyingi, dhabibu ambazo haziwezi kuondoa dhambi.
|
12 |
Lakini Kristo alitoa dhabihu moja tu kwa ajili ya dhambi, dhabihu ifaayo milele, kisha akaketi upande wa kulia wa Mungu.
|
13 |
Huko anangoja mpaka adui zake watakapowekwa kama kibao chini ya miguu yake.
|
14 |
Basi, kwa dhabihu yake moja tu, amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wanaotakaswa dhambi zao.
|
15 |
Naye Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema:
|
16 |
"Hili ndilo agano nitakalofanya nao, katika siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao."
|
17 |
Kisha akaongeza kusema: "Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu."
|
18 |
Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa dhabihu za kuondoa dhambi.
|
19 |
Basi, ndugu, kwa damu ya Yesu tunapewa moyo thabiti wa kuingia Mahali Patakatifu.
|
20 |
Yeye ametufungulia njia mpya na yenye uzima kupitia lile pazia, yaani kwa njia ya mwili wake mwenyewe.
|
21 |
Basi, tunaye kuhani maarufu aliye na mamlaka juu ya nyumba ya Mungu.
|
22 |
Kwa hiyo tumkaribie Mungu kwa moyo mnyofu na imani timilifu, kwa mioyo iliyotakaswa dhamiri mbaya, na kwa miili iliyosafishwa kwa maji safi.
|
23 |
Tushikilie imara tumaini lile tunalokiri, maana Mungu aliyefanya ahadi zake ni mwaminifu.
|
24 |
Tujitahidi kushughulikiana kwa ajili ya kuongezeana bidii ya kupendana na kutenda mema.
|
25 |
Tusiache ile desturi ya kukutana pamoja, kama vile wengine wanavyofanya. Bali tunapaswa kusaidiana kwani, kama mwonavyo, Siku ile ya Bwana inakaribia.
|
26 |
Maana, tukiendelea kutenda dhambi makusudi baada ya kufahamu ukweli, hakuna dhabihu iwezayo kutolewa tena kwa ajili ya kuondoa dhambi.
|
27 |
Linalobaki ni kungojea tu kwa hofu hukumu ya Mungu na moto mkali utakaowaangamiza wote wanaompinga.
|
28 |
Mtu yeyote asiyeitii Sheria ya Mose, huuawa bila ya huruma kukiwa na ushahidi wa watu wawili au watatu.
|
29 |
Je, mtu yule anayempuuza Mwana wa Mungu na kuidharau damu ya agano la Mungu iliyomtakasa, mtu anayemtukana Roho wa Mungu, anastahili kupata adhabu kali ya namna gani?
|
30 |
Maana tunamfahamu yule aliyesema, "Mimi nitalipiza kisasi, mimi nitalipiza," na ambaye alisema pia, "Bwana atawahukumu watu wake."
|
31 |
Kuanguka mikononi mwa Mungu aliye hai ni jambo la kutisha mno!
|
32 |
Kumbukeni yaliyotokea siku zile za kwanza mlipoangaziwa mwanga wa Mungu. Ingawa siku zile mlipatwa na mateso mengi, ninyi mlistahimili.
|
33 |
Mara nyingine mlitukanwa na kufedheheshwa hadharani; mara nyingine mlikuwa radhi kuungana na wale walioteswa namna hiyohiyo.
|
34 |
Mlishiriki mateso ya wafungwa, na mliponyang`anywa mali yenu mlistahimili kwa furaha, maana mlijua kwamba mnayo mali bora zaidi na ya kudumu milele.
|
35 |
Basi, msipoteze uhodari wenu, maana utawapatieni tuzo kubwa.
|
36 |
Mnahitaji kuwa na uvumilivu, ili mweze kufanya anayotaka Mungu na kupokea kile alichoahidi.
|
37 |
Maana kama yasemavyo Maandiko: "Bado kidogo tu, na yule anayekuja, atakuja, wala hatakawia.
|
38 |
Lakini mtu wangu aliye mwadilifu ataamini na kuishi; walakini akirudi nyuma, mimi sitapendezwa naye."
|
39 |
Basi, sisi hatumo miongoni mwa wale wanaorudi nyuma na kupotea, ila sisi tunaamini na tunaokolewa.
|