| Chapter 3 |
1 |
Oneni basi, jinsi Baba alivyotupenda mno hata tunaitwa watoto wa Mungu! Na kweli, ndivyo tulivyo. Ndiyo maana ulimwengu haututambui sisi, kwani haumjui Mungu.
|
2 |
Wapenzi wangu, sisi ni watoto wa Mungu sasa, lakini bado haijaonekana wazi jinsi tutakavyokuwa. Lakini tunajua kwamba wakati Kristo atakapotokea, tutafanana naye kwani tutamwona vile alivyo.
|
3 |
Basi, kila mtu aliye na tumaini hili katika Kristo, hujiweka safi kama vile Kristo alivyo safi kabisa.
|
4 |
Kila mtu atendaye dhambi anavunja sheria ya Mungu, maana dhambi ni uvunjaji wa sheria.
|
5 |
Mnajua kwamba Kristo alikuja kuziondoa dhambi zetu, na kwamba kwake hamna dhambi yoyote.
|
6 |
Basi, kila aishiye katika muungano na Kristo hatendi dhambi; lakini kila mtu atendaye dhambi hakupata kamwe kumwona, wala kumjua Kristo.
|
7 |
Basi, watoto wangu, msikubali kupotoshwa na mtu yeyote. Mtu atendaye matendo maadilifu ni mwadilifu kama vile Kristo alivyo mwadilifu kabisa.
|
8 |
Lakini atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi ametenda dhambi tangu mwanzo. Lakini Mwana wa Mungu alikuja duniani kuiharibu kazi ya Ibilisi.
|
9 |
Kila aliye mtoto wa Mungu hatendi dhambi, maana anayo hali ya kimungu ndani yake; hawezi kutenda dhambi kwa sababu yeye ni mtoto wa Mungu.
|
10 |
Lakini yeyote asiyetenda mambo maadilifu, au asiyempenda ndugu yake, huyo si mtoto wa Mungu. Hiyo ndiyo tofauti iliyoko kati ya watoto wa Mungu na watoto wa Ibilisi.
|
11 |
Na, ujumbe mliousikia tangu mwanzo ndio huu: Tunapaswa kupendana!
|
12 |
Tusiwe kama Kaini ambaye, kwa kuongozwa na yule Mwovu, alimuua ndugu yake. Na, kwa nini alimuua? Kwa sababu matendo yake yalikuwa maovu, lakini yale ya ndugu yake yalikuwa mema!
|
13 |
Basi, ndugu zangu, msishangae kama ulimwengu unawachukia ninyi.
|
14 |
Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo na kuingia katika uzima kwa sababu tunawapenda ndugu zetu. Mtu asiye na upendo hubaki katika kifo.
|
15 |
Kila anayemchukia ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua kwamba muuaji yeyote yule hana uzima wa milele ndani yake.
|
16 |
Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu.
|
17 |
Basi, mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona ndugu yake ana shida, lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma, anawezaje kusema kwamba anampenda Mungu?
|
18 |
Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe upendo wa kweli na wa vitendo.
|
19 |
Hivyo ndivyo tuwezavyo kuwa na hakika kwamba sisi ni watu wa ukweli; na hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu.
|
20 |
Kwa maana, hata kama dhamiri yetu yatuhukumu, twajua kwamba Mungu ni mkuu zaidi kuliko dhamiri, na kwamba yeye ajua kila kitu.
|
21 |
Wapenzi wangu, kama dhamiri yetu haina lawama juu yetu, basi, twaweza kuwa na uthabiti mbele ya Mungu,
|
22 |
na twaweza kupokea kwake chochote tunachoomba, maana tunazitii amri zake na kufanya yale yanayompendeza.
|
23 |
Na, amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Kristo, na kupendana kama alivyotuamuru.
|
24 |
Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na Mungu na Mungu anaishi katika muungano naye. Kwa njia ya Roho ambaye Mungu ametujalia, sisi twajua kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi.
|